Friday, August 21, 2015

AJINYONGA BAADA YA KUKATALIWA NA MCHUMBA WAKE AMBAYE WALIKUWA WAFUNGE NDOA 28.08.2015


Na Juhudi  Felix-KYERWA

Mtu mmoja  mkazi  wa  Kitongoji cha  Kishanda B Kijiji cha Kyerwa   Kata  ya  Kyerwa  wilayani  Kyerwa  mkoani  Kagera  amekutwa amejinyonga  nyumbani  kwake  na  kuacha  ujumbe unaelezea sababu  za  kujinyonga  kwake   kuwa  ni  kukataliwa kwa  mchumba  wake  waliokuwa  wanatarajia  kufunga  ndoa  Agosti 28  mwaka  huu.

Akithibitisha tukio  hilo  jana  mwenyekiti  wa  kitongoji hicho Ibrahimu  Paschal alisema  kuwa  aliyejinyonga  ni Sabinus  Gabriel  miaka (30) na alitumia  kamba  ya  katani  aliyoifunga  kwenye  dari    ya  nyumba  yake.

Alisema  marehemu  aliacha  ujumbe aliouandika  ukielezea   sababu  zilizopelekea  kuchukua  uamuzi  huo  wa  kujiua  kuwa  ulitokana  na  kukataliwa  na  binti  aliyekuwa  anamchumbia  na  taratibu  zilikuwa  zimeishakamilika  na  mchumba  wake  huyo  kubadili  maamuzi  ghafla  na  kumweleza  hamtaki  tena  kwasababu  amempata  mwingine.

Aliyejinyonga  alitarajia  kufunga  ndoa  Agosti 28  mwaka  huu  ambapo  wana  ndugu  walieleza  kuwa  taratibu  za  kutoa  mahali  zilikuwa  zimeishafuatwa  ambapo  Jumatatu  ya  Agosti 17  mwaka  huu  baadhi  ya  vitu  vilipelekwa  kwa  wazazi  wake  na  binti.




Mwenyekiti  huyo  alisema  kuwa  tukio  hilo  la  watu  kujinyonga  katika  kijiji  hicho  ni  la  pili  ndani  ya  wiki  mbili  kwani  kuna  baba   mmoja alijinyonga  baada  ya  mke  wake  kuondoka  na  kurudi  kwa  wazazi  wake  huku  akihaidi  kutorudi   kwake  na  ndoa  yao  haipo  tena  kutokana  na  kile  kilichodaiwa  ni  kuwepo  migogoro  ya  muda  mrefu ndani  ya  familia  hiyo.

Aidha  Mzazi wa marehemu Gabriel  Rubinduka  alieleza kusikitishwa na tukio  la  kifo cha mtoto wake ambaye walitarajia kumfanyia sherehe  kama walivyokuwa wameazimia kutokana na maandalizi yaliyokuwa yamefanyika katika familia yao.

“Ni majonzi  makubwa  kweli  familia  tulishajiandaa  kumwandalia  sherehe  kubwa  lakini  hili lililomtokea  sijui  kama  ni  mipango  ya  Mungu  ila  yote  tunamwachia  aliyetuumba  na  kilichobakia  ni  kuendelea  kumwombea  pumziko  la  Amani”Alisema  Gabriel
Binti  aliyekuwa  anachumbiwa  Jovitha  Novath   alipofuatwa  na  waandishi wa  habari  kuelezea   mkasa  huo  kama  ujumbe  ulioachwa  na  marehemu  kama  una  ukweli  ndani  yake  hakuwa   tayari  kuzungumzia  tukio  hilo.

Kwa  upande  wake  Novath  Kalekona  ambaye  ni  mzazi  wa  binti  aliyekuwa  anachumbiwa  alikiri  kuwa  ni  kweli  binti  yake  kuchumbiwa  na  huyo  aliyejinyonga  na  kusema  kuwa  ni kweli  baadhi ya  mali  alikwishapokea  kutoka  kwa  wazazi  wake  na  marehemu.

“Ni  kweli   wazazi  wa  marehemu  walileta  mali  ambazo  kwa  makubaliano  ambayo  ni  taratibu  ambazo  ni  utamaduni  wetu  lazima  kuzitimiza  na  walikuwa  kwangu  jumatatu  ya  Agosti 17  mwaka  huu  lakini  hili  la  kujinyonga  limenishutua  hata  mimi na  hatukujua kama  kuna  hali  kama  hiyo  maana  walikuwa  wakipendana  kweli”Alisema  Kalekona

Jeshi  la  polisi  wilayani  Kyerwa  wameruhusu  mwili  wa  marehemu  kuzikwa  baada  ya  uchunguzi  wa  kitabibu  uliofanywa  na  mganga mfawidhi   kutoka  Zahanati  ya  Kimuli Braisoni  Katabaro.

No comments:

Post a Comment